MPANGILIO wa alama mpya za kufaulu
kwa wahitimu wa kidato cha sita waliohitimu mwaka jana, ambao matokeo ya
mitihani yao yanaweza kutangazwa wakati wowote kuanzia sasa, unadaiwa
kuzua aibu na kama si uamuzi uliotajwa bungeni wa matumizi ya alama za
ufaulu za zamani, matokeo hayo yangeibua aibu kama ilivyojitokeza kwa
kidato cha nne, 2012.
Kwa mujibu wa vyanzo vyetu vya habari
kutoka Baraza la Taifa la Mitihani (NECTA) ambalo linaendelea kupanga
matokeo hayo ya kidato cha sita kwa kuzingatia alama za zamani kama
ambavyo taarifa ya awali ya Tume iliyoundwa na Waziri Mkuu, Mizengo
Pinda, ilivyosomwa bungeni hivi karibuni, hali ingekuwa mbaya zaidi
katika ufaulu kwa wanafunzi wa kidato cha sita kiasi cha kuweza kutishia
uhai wa vyuo vikuu nchini kukosa wanafunzi wa kutosha.
“Hali ilikuwa mbaya sana kama alama
za kufaulu zingeachwa zitumike zile mpya na si za zamani. Vyuo vikuu
nchini visingeweza kupata wanafunzi wa kutosha.
"Tatizo hapa si uwezo wa wanafunzi moja kwa moja katika kumudu mitihani bali ni kufanywa kwa mabadiliko ya alama bila kuwaandaa.
" Alama hizi zilipaswa kuanza
kutumika na wanafunzi wapya, yaani kama wanaanza kidato cha kwanza wawe
wanapewa mitihani ya kupimwa kwa kuzingatia alama mpya na waendelee nazo
hadi mitihano yao ya mwisho.
“Na hivyo hivyo kwa wanafunzi wa
kidato cha sita. Alama hizi mpya zinapaswa kutumika kwako kuanzia wakiwa
kidato cha tano mara wanapoanza shule, kila mitihani wanayopewa
isahihishwe na kupangiwa alama kwa kutumia hizi alama mpya,” kinaeleza
chanzo chetu cha habari kutoka NECTA.
Kwa mujibu wa mabadiliko hayo ya
alama, alama mpya zilizokuwa zimetumika awali ni daraja F kuanzia 34
hadi sifuri; badala ya alama hiyo F kuanzia 20 hadi 0; daraja D kwa
kuzingatia alama mpya linapaswa kuanzia 35 tofauti na awali, yaani alama
21.
Taarifa zaidi zinabainisha ya kuwa,
kati ya sababu za kuchelewa kutangazwa kwa matokeo ya kidato cha sita
tofauti na muda uliotarajiwa yaani mwanzoni mwa Mei, ni pamoja na
upangaji upya matokeo hayo, ikiwa ni tofauti na ilivyokuwa kwa kidato
cha nne ambapo matokeo yalitangazwa na kisha kufutwa ili kuyapanga upya
kwa kutumia alama za zamani.
Lakini alipoulizwa kuhusu masuala
hayo ndani ya NECTA, Ofisa Habari wa Taasisi hiyo nyeti nchini, John
Nchimbi alisema; “Kwa sasa niseme tu kwamba mchakato wa kuandaa matokeo
ya kidato cha sita unaendelea, siwezi kusema lini hasa utakamilika
lakini nina uhakika ni katika muda muafaka.”
Kuhusu matokeo ya kidato cha sita
kucheleweshwa kutokana kupangwa upya ili kupunguza idadi ya waliofeli
kutokana na matumizi ya alama mpya za kufaulu, Nchimbi anasema; “Unajua
haya maagizo haya ya bungeni (kupanga matokeo kwa kuzingatia alama za
zamani) yamekuja wakati mchakato wa kuandaa matokeo ulikwishaanza. Kwa
hiyo baada ya maagizo ilibidi kufanya kazi hiyo tena kwa kufuata maagizo
hayo.”
Hata hivyo, hakuweka bayana kama
matokeo ya awali kabla ya maagizo ya Serikali yaliyotolewa bungeni
kutumia alama za zamani yamewafanya wanafunzi wengi kufeli na badala
yake akasema; “Hilo siwezi kulizungumzia kwa sababu mchakato wa matokeo
hayo haukuwa umefika mwisho. Takwimu rasmi hazikuwa zimekamilishwa. Kwa
hiyo si sahihi kusema rasmi walifeli.”
Lakini wakati hali ikiwa hivyo kwa
upande wa matokeo yanayotarajiwa ya kidato cha sita, taarifa zaidi
zinabainisha ya kuwa, baada agizo la serikali la kufuta na kurejewa upya
kwa matokeo ya kidato cha nne mwaka 2012, takriban wanafunzi 50,000
wamepata unafuu katika matokeo yao tofauti na awali.
Awali, kwa kuzingatia matokeo ya
kidato cha nne mwaka jana yaliyotangazwa Februari, mwaka huu jijini Dar
es Salaam, Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi Dk. Shukuru Kawambwa,
jumla ya watahiniwa 126,847 tu kati ya watahiniwa 397,136 waliofanya
mtihani huo walifaulu.
Katika matokeo hayo idadi ya
wasichana waliofaulu ilitajwa kuwa ni 46,181 wakati wavulana waliofaulu
ikiwa wanafunzi 80,686 na idadi ya watahiniwa wa kujitegemea waliofaulu
ni 16,112 kati yao watahiniwa 61,001 waliofanya mtihani wasichana ni
6,7751 na wavulana 9,361.
Katika matokeo hayo watahiniwa
waliopata daraja la kwanza ni 1,641, daraja la pili 6,453 na daraja la
tatu ni 15,426, wakati waliopata sifuri ni 240,903 lakini kwa kuzingatia
taarifa za vyanzo vyetu ndani ya Baraza, idadi hiyo itabadilika kwa
sababu ya alama kuongezwa kwa watahiniwa hao wa mwaka 2012.
Lakini matokeo hayo yalitangazwa
pamoja na vituko walivyofanya baadhi ya wanafunzi, vikiwamo vituko vya
kuandika matusi kwenye karatasi za majibu ya mitihani na kutokana na
makosa hayo, watahiniwa 789 walifutiwa mitihiani yao.
Source;raia mwema
0 comments:
Post a Comment