Serikali imetoa tamko bungeni kuhusu mauaji ya raia mikononi mwa polisi
ikieleza kuwa sheria ya kanuni ya adhabu inaruhusu kutumia nguvu za
kadiri hata kiasi cha kusababisha madhara au kifo.
Kauli
hiyo imekuja siku chache baada ya Waziri Mkuu, Mizengo Pinda kunukuliwa
bungeni akiwataka polisi kuwashughulikia kwa kuwapiga watu wote
wanaokaidi kutii sheria.
“…Nasema wapigwe tu, maana tumechoka sasa,” alisema Pinda alipojibu maswali ya papo hapo Alhamisi iliyopita
Akisoma tamko hilo bungeni jana, Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani, Pereira
Ame Silima alisema kuwa kifungu cha 18(B) na 18(C) cha Sheria ya Kanuni
ya Adhabu kinatoa uwezo kisheria wa kutumia nguvu za kadiri hata
ikibidi kiasi cha kusababisha madhara au kifo katika mazingira ya
kisheria.
Aliyataja mazingira hayo kuwa ni pamoja na kuokoa
uhai wa mtu mwingine, kuzuia madhara makubwa ya mwili yasitokee kwake au
kwa mtu mwingine na kumzuia mtu anayetenda tendo ovu la kubaka au
kunajisi mtoto au kufanya vitendo kinyume na maumbile.
Pia
kumzuia mtu anayevunja nyumba usiku au unyang’anyi wa kutumia silaha au
kuchoma nyumba moto au kufanya kitendo chochote kinachohatarisha uhai wa
mtu au mali.
Alieleza kuwa Kifungu cha 18 na 18(A) cha
Sheria ya Adhabu Sura namba16 iliyofanyiwa mapitio mwaka 2002, kinampa
haki mtu yeyote akiwemo askari kujilinda, kumlinda mtu mwingine, kulinda
mali yake au mali ya mtu mwingine ikiwemo ya Serikali na taasisi zake,
ambayo iko chini ya uangalizi wake kisheria.
Kauli hiyo ya
Serikali kuhusu mauaji ya raia mikononi mwa polisi, ilitolewa ikiwa ni
ufafanuzi wa jibu la swali la nyongeza lililoulizwa bungeni Mei 28,2013
na Rashir Ally Abdalah (Tumbe-CUF), ambapo Silima alisema mauaji
yanayofanywa na askari polisi ni mauaji ya kisheria.
Kutokana na
kauli hiyo, Mbunge wa Wawi, Hamad Rashi Mohammed aliomba mwongozo wa
spika kupata ufafanuzi wa kauli hiyo, na jana Silima kutoa kauli ya
Serikali kujibu mwongozo huo.
“Ikumbukwe pia kuwa, kifungu cha 29
cha Sheria ya Jeshi la Polisi na Polisi wasaidizi Sura322, pamoja na
Kanuni za Kudumu za Utendaji za Jeshi la Polisi Na274, vinampa haki ya
kisheria askari polisi kubeba na kutumia silaha za moto ikiwamo bunduki
na mabomu katika utekelezaji wa majukumu yake ya kila siku..,”alisema
Silima.
Alifafanua kwamba katika kutafsiri sheria, kanuni na
taratibu mbalimbali ikiwamo alizozitaja, mahakama katika nyakati tofauti
imetoa msimamo wa kisheria juu ya suala hilo.
Akitoa mfano
alisema: “Mathalan katika kesi ya Seif Mohamed Senzagala dhidi ya
Jamhuri ya mwaka 1994 kama ilivyonukuliwa na Tanzania Law Report ukurasa
wa 122, ambapo mshitakiwa (mwomba rufaa) alimjeruhi kwa panga
mlalamikaji ambaye alimfuata nyumbani kwake na kuanza kumshambulia.”
Alisema
katika kesi hiyo,mahakama ya rufaa pamoja na kuridhia uamuzi wa
mahakama ya awali wa kumtia hatiani kwa kutumia nguvu kupita kiasi,
ilibainisha kuwa mshtakiwa hakustahili adhabu kwani alitenda kosa lile
wakati akijihami dhidi ya mashambulizi toka kwa mlalamikaji.
“Kwa
msingi huo, tarehe 28 Mei, 2013 wakati nikijibu swali Na 290, nilitumia
maneno ‘mauaji yanayofanywa kisheria’ nikimaanisha mauaji yanayotokea
katika mazingira niliyoeleza..,”alisema Silima.
Hata hivyo
alisema siyo nia ya Serikali kuhalalisha vitendo vya matumizi mabaya ya
silaha ambavyo vinaweza kufanywa na askari wasio waadilifu.
Alibainisha
kuwa Jeshi la Polisi litaendelea kutekeleza majukumu yake kwa mujibu wa
sheria, kuheshimu haki za raia na kutumia busara kutatua migogoro.
Hata
hivyo, Kambi rasmi ya Upinzani Bungeni imelaani kauli ya Serikali
kuhusu mauaji ya raia mikononi mwa polisi iliyoitoa jana na kueleza kuwa
haikubaliani nayo kwa kuwa inatoa baraka kwa polisi kuendeleza mauaji
ya raia.
Akizungumza na mwandishi wetu baada ya kikao cha bunge
kuahirishwa, Waziri Kivuli wa Mambo ya Ndani wa kambi hiyo rasmi, Vicent
Nyerere alisema kauli hiyo ingekuwa na uthabiti kama askari polisi
wangekuwa waadilifu.
“Kauli ingekuwa thabiti kama polisi
wangekuwa waadilifu. kabla ya kutoa kauli hiyo, Serikali ilitakiwa
kuchuja miongoni mwa askari wa jeshi la polisi, wa ngazi zote na
kuwaondoa wasio waaadilifu ndipo wakatoa kauli hiyo wananchi wataielewa
Serikali,”alisema Nyerere ambaye pia ni Mbunge wa Musoma Mjini(Chadema).
Kwa
upande wake, Mbunge wa Ole, (CUF) Rajab Mbarouk Mohammed akizungumzia
kauli hiyo ya Serikali alisema kuwa majibu ya Naibu Waziri wa Mambo ya
Ndani, Pereira Ame Silima ni ya kisiasa.
Alisema kwamba kauli
hiyo ni mwendelezo wa kauli iliyotolewa Alhamisi iliyopita na Waziri
Mkuu,Mizengo Pinda akiwataka pilisi kuwashughulikia kwa kuwapiga watu
wote watakaokaidi kutii sheria.
“Hakuna mwenye haki ya kuua,
kuua ni kuua tu. Mahakama pekee ndiyo ina haki ya kuhukumu kifo baada ya
kumtia hatiani mshtakiwa husika. Lakini kuwa polisi wanafundishwa utii,
siyo kuua,”alisema Rajab.
Alifafanua kuwa kazi ya polisi ni kulinda raia na mali zao na kwamba kuruhusiwa kujihami haimaanishi kuua raia.
Nao
Wabunge Aeshi Hilaly na Aly Keissy walisema ni vizuri raia wakatii
mamlaka iliyopo na kutekeleza utii wa sheria bila shuruti.
Mbunge wa Kilwa Kaskazini, Murtaza Mangungu alisema: “Maoni yangu haki za watuhumiwa lazima ziheshimiwe.”
Rais
wa Chama cha Wanasheria Tanganyika, (TLS), Francis Stola alisema hakuna
sheria inayompa mamlaka askari polisi kutumia nguvu za ziada ikiwemo
kupiga raia pindi anapotekeleza majukumu yake,isipokuwa tu anaweza
kutumia nguvu kiasi iwapo raia anayekabiliana naye anaonyesha vitendo
vya kukaidi amri ama kuhatarisha usalama.
Stola ambaye
alikuwa akitoa ufafanuzi wa kisheria kuhusiana na kauli bungeni alisema
kuwa kwa kufuata sheria polisi haruhusiwi kupiga raia. “ Ukisoma sheria
hakuna mahala utakuta kuna neno limeandika piga…. Askari polisi
anachoweza kufanya ni arrest(kamata) na siyo vinginevyo, hana mamlaka
kabisa ya kupiga raia”
Alisema sheria imetamka wazi kuwa
kunapojitokeza hali yoyote inayopaswa kdhibitiwa na vikosi vya ulinzi,
nguvu inayopaswa kutumika ni ile ya kawaida na kwamba kitendo cha
kutumia risasi za moto ama kupiga raia ni ukiukwaji wa sheria za nchi.
Alisema
polisi anapaswa kutoa mwongozo kwa raia kumwelekeza jambo la kufanya
iwapo kunajitokeza hali ya sintofahamu,lakini hapaswi kutumia nguvu
kupita kiasi ikiwemo kuwapiga raia
“ Sheria inasema wazi kwamba
panapojitokeza hali yoyote korofi, polisi wanatakiwa kutumia nguvu ya
kawaida tu kukabiliana na hali hiyo na wala siyo kutumia silaha za moto…
silaha za moto zinaweza kutumika tu iwapo kunajitokeza tukio ambalo
linaweza kuhatarisha usalama wa maisha ama mali isipotee” alisema
Kuhusu
wananchi kufanya maandamano, rais huyo alisema maandamano ni haki ya
msingi ya kila raia,lakini yanafanyika katika utaratibu maalumu. “
maandamano ni haki ya kila raia lakini panapaswa kuwa na utaratibu
maalumu…. Kama kunajitokeza maandamano ambayo hayana utaratibu polisi
wanapaswa kutumia reasonable force (nguvu ya kawaida) kudhibiti
maandamano hayo na wala siyo kutumia nguvu za ziada.