Dar es Salaam. Siku moja baada ya
Rais wa Marekani, Barack Obama kuondoka nchini, maisha kwa wakazi wa Dar
es Salaam yamerejea katika hali ya kawaida, huku baadhi ya
wafanyabiashara na ombaomba wakirejea kwa kasi maeneo yaliyosafishwa
wakati wa ujio huo.
Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam
ilianzisha operesheni maalumu ya usafi kabla na wakati wa ujio wa Obama,
hatua iliyopokewa kwa mtazamo tofauti na wakazi hao.
Timu ya Mwananchi iliyovinjari kona
mbalimbali za Dar es Salaam jana, ilishuhudia wafanyabiashara wakirudi
huku wengine wakijenga upya vibanda vilivyobomolewa.
Kwa nyakati tofauti, baadhi ya
wafanyabiashara hao, walisema changamoto za maisha zinazowakabili ndizo
zimewasukuma kurejea, kwa sababu hawana kazi wala sehemu nyingine ya
kufanyia biashara zao.
Kituo cha Mabasi Mwenge, kulikuwa na wafanyabiashara wachache walioanza kurudi taratibu kwa kuvizia.
Mwananchi ilikutana na ombaomba
kadhaa Barabara ya Sam Nujoma na ile inayoelekea Kiwanda cha CocaCola
Kwanza Mikocheni, huku polisi waliokuwa makutano hayo wakiwaangalia bila
kufanya chochote.
Wafanyabiashara hao walisema wameamua kuendelea kufanya biashara zao kutokana na hali ngumu ya maisha inayowakabili.
Katika maeneo ya Ubungo,
wafanyabiashara ndogondogo walionekana kuendelea na biashara hususan
pembezoni mwa barabara, Ubungo Darajani na ndani ya Kituo cha Daladala
cha Ubungo.
Hata hivyo, licha ya kuendelea na
biashara hizo, baadhi yao wameonyesha wasiwasi kufungua kwenye maeneo
hayo waliyofukuzwa awali, kwani hakuna tamko lililowaruhusu kuendelea.
Mmoja wa wafanyabiashara hao, Jabir
Hamis, alisema: “Nashukuru kumalizika kwa ziara ya Rais Obama nchini,
kwani tuna siku mbili hatujafanya biashara.”
Wafanyabiashara wengine waliorudi
maeneo ya Ubungo, ni wale wanaofanya biashara za nguo katika makutano ya
Barabara za Mandela, Sam Nujoma na Morogoro na bodaboda wanaoegesha
Kituo cha Tanesco.
Tabata Relini karibu na Ofisi za
Mwananchi Communications Limited (Ltd), wafanyabiashara ndongondogo
waliovunjiwa vibanda, walianza kujenga mabanda yao na kurudi kwa
kasi.“Sisi bwana, tumerudi kwa sababu hapa tunajipatia kula. Ni kweli
tupo kinyume cha sheria, lakini hatuna jinsi hapa ndipo tunapopata
riziki zetu, nasomesha watoto kwa kazi hii ya mamalishe,” alisema mmoja
wa mamalishe ambaye hakutaka kutajwa.
Maeneo ya Buguruni, wafanyabiashara
wanaopanga bidhaa zao pembezoni mwa barabara, walirejea na kuendelea na
shughuli zao kawaida.
Wauza nguo za mitumba wamerejea eneo
la Bakhresa, walisema wao wanaamini waliondolewa kupisha msafara wa
Obama, baada ya hapo wanaendelea.
Hali ya uchafu nayo ilionekana
kurejea eneo hilo, mifuko ya plastiki na makaratasi yalionekana kuzagaa
barabarani ambayo Jumanne ilikuwa iking’aa kwa usafi.
Maeneo ya Kariakoo kwenye makutano ya
Barabara ya Uhuru na Msimbazi, lilionekana katika hali ya usafi na
kuvutia kama ilivyokuwa wakati wa ujio wa Obama, ingawa wafanyabiashara
walianza kurudi kwa kuvizia mgambo.
Takriban wiki moja kuelekea ujio wa
Obama, maeneo mbalimbali ya katikati ya Dar es Salaam na pembezoni,
yalikuwa katika hali ya usafi na wafanyabiashara waliokuwa wakipanga
bidhaa pembezoni mwa maeneo yasiyo rasmi waliondolewa.
0 comments:
Post a Comment